You are here

Unyenyekevu katika swala

×

Error message

Deprecated function: Function create_function() is deprecated in views_php_handler_field->pre_render() (line 202 of /var/www/drupal7-websites/sites/all/modules/contrib/views_php/plugins/views/views_php_handler_field.inc).

Unyenyekevu ndani ya swala ndio hasa swala yenyewe, na ndio msingi wake. Maana yake ni moyo wangu kutambua kuwa nipo mbele ya Allah ndani ya swala kwa kuhisi unyenyenyekevu na udhaifu, nikizitilia maanani aya, dua na nyiradi ninazozisema.

Unyenyekevu ni katika ibada bora kabisa na ni katika utii uliotukuka sana. Kwa sababu hii, Allah ametilia mkazo ndani ya kitabu chake kuwa unyenyekevu ni katika sifa za waumini, kama alivyosema kuwa: «Hakika, Waumini wamefaulu, ambao wao katika swala zao ni wanyenyekevu». (Sura Almuuminuun, aya 1-2).

Mwenye kuwa na na unyenyekevu katika swala ataonja ladha ya ibada na iman. Kwa sababu hiyo, Mtume wa Allah,swallalahu alayhi wasalam, alikuwa akisema kuwa: «Na burudani yangu imewekwa katika  swala». (Annasai, Hadithi Na. 3940). Burudani ina maana ya kiwango cha juu cha furaha, faraja, kuliwazika na kustareheka.

Thawabu katika swala zinapatikana kwa kadiri ya unyenyekekevu ndani yake.

Nyenzo zinazosaidia kuwa na unyenyekevu ndani ya swala

Kuna nyenzo nyingi zinazosaidia kupata unyenyekevu wakati wa kuswali. Miongoni mwa nyenzo hizo ni hizi: 

  1. Kujiandaa na kujitayarisha kwa ajili ya swala: 

Hilo linatimia kwa kwenda mapema msikitini kwa wanamume, kufanya ibada za sunna zilizo kabla ya swala, kuvaa nguo nzuri za heshima, kwenda msikitini katika hali ya utulivu na unyenyekevu.

  1. Kujiepusha na vitu vyote vyenye kushughulisha na kusumbua:

Mtu hatakiwi kuswali hali ya kuwa mbele yake kuna picha au vitu vinavyoshughulisha, na wala asiingie katika swala hali ya kuwa anasikia sauti zinazomshughulisha. Pia hatakiwi kuingia katika swala huku akiwa amebanwa na haja, au akiwa na njaa au kiu na mbele yake kuna chakula au kinywaji. Hatua zote hizo zimewekwa ili akili ya anayeswali iwe safi na aweze kushughulika na jambo kubwa lililoko mbele yake na ambalo ni swala yake na kuzungumza kwake na Mola wake. 

  1. Utulivu katika swala:

Mtume,swallalahu alayhi wasalam, alikuwa mtulivu wakati akirukuu na kusujudu mpaka kila kiungo kinakaa mahali pake. Alimuamrisha mtu ambaye alikuwa hajui kuswali vizuri awe mtulivu katika vitendo vyote vya swala. Amekataza kuharakisha na akafananisha kitendo hicho na papara ya kunguru.  

Mtume,swallalahu alayhi wasalam, amesema kuwa: «Mwizi mbaya kabisa kuliko watu wote ni yule anaye iba katika swala yake. Swahaba wakauliza: Ewe Mtume wa Allah: Vipi mtu anaiba katika swala yake? Mtume akajibu: Ni yule mtu asiyetimiza rukuu yake na sijida yake». (Ahmad, hadithi Na. 22642).

Mtu ambaye hana utulivu katika swala yake hawezi kuwa na unyenyekevu, kwa sababu haraka huondosha unyenyekevu, na papara ya kunguru huondosha thawabu.

  1. Mtu kuchunga heshima mbele ya Mola wake:

Mtu anatakiwa akumbuke ukubwa na utukufu wa Muumba, na pia akumbuke udhaifu na udhalili wake, na kwamba anasimama mbele ya Mola wake akizungumza naye na akimuomba kwa unyenyekevu, unyonge na udhalili. Anatakiwa akumbuke thawabu ambazo Allah amewaandalia Waumini, na adhabu ambazo amewaandalia Makafiri huko Akhera. Pia akumbuke jinsi atakavyo simama mbele ya Mola wake huko Akhera.

Muumini akiwa katika hali hii ndani ya swala yake atakuwa kama wale ambao Allah amewasifu katika kitabu chake kwamba wanaamini kuwa watakutana na Mola wao. Allah Mtukufu amesema kuwa: «Na kwa yakini kabisa, hiyo swala ni jambo kubwa (zito) isipokuwa kwa wenye unyenyekevu. Ambao wanadhani (wanaamini) kuwa  watakutana na Mola wao, na kwamba wao watarejea kwake». (Sura Albaqara, aya 45-46)

Mwenye kuswali akitambua kuwa Allah anamsikia, anampa (neema mbali mbali) na anamjibu (maombi yake) atapata unyenyekevu kwa kiasi cha kutambua kwake.

  1. Kuzingatia aya zinazosomwa na nyiradi nyingine za swala, na kuzifanyia kazi:

Qur`ani imeshushwa ili izingatiwe. «(Hiki) Ni kitabu chenye baraka, tumekiteremsha kwako ili watu wazizingatie aya zake, na wenye akili wapate onyo».(Sura Saad, aya 29). Uzingatiaji haupatikani isipokuwa tu kwa kujua maana ya aya, nyiradi na dua zinazosomwa.  Hapo, itawezekana kwake kufikiria hali yake na uhalisia wake kwa upande mmoja, na kufahamu maana ya aya na nyiradi hizo kwa upande mwingine. Kutokana na hilo, utapatikana unyenyekevu na kuguswa, na pengine hata macho yake yakabubujikwa na machozi. Haziwezi kumpitia aya bila ya kuguswa nazo, kama kwamba hasikii wala haoni.  Allah Mtukufu amesema kuwa: «Na wale ambao wakikumbushwa aya za Mola wao hawajifanyi hamnazo (hawazipuuzi)». (Sura Alfurqan, aya 73).

Mwongozo Mwepesi wa Muislam

Mtandao wa Mwongozo Mwepesi wa Muislam ni kitabu cha Mtandaoni cha kitabu asili ‘Mwongozo Mwepesi wa Muislam’ ambacho ni moja ya mradi wa Kampuni ya Mwongozo wa Kisasa na kimetolewa katika Lugha Zaidi ya 15 na maudhui yake yameambatana na ujuzi mkubwa wa kimtandao katika kufikisha.

الدليل المعاصر