You are here

Ni mali zipi ambazo inawajibika kuzitolea zaka?

×

Error message

Deprecated function: Function create_function() is deprecated in views_php_handler_field->pre_render() (line 202 of /var/www/drupal7-websites/sites/all/modules/contrib/views_php/plugins/views/views_php_handler_field.inc).

Zaka sio wajibu katika vitu ambavyo Muislamu anavimiliki ili kufaidika navyo moja kwa moja yeye mwenyewe, kama vile nyumba yake anayoishi hata kama itakuwa na thamani kubwa kiasi gani, wala gari lake analotumia  hata kama ni la kifahari kiasi gani. Hivyo hivyo nguo zake, chakula chake na vinywaji vyake.

Allah amewajibisha zaka katika aina fulani ya mali ambazo zina sifa ya kwamba hazipo katika mahitaji ya matumizi yake ya lazima, na ambazo kwa kawaida ya mali hizo zinakuwa na kuongezeka, kama hizi zifuatazo:

 1. Dhahabu na Fedha ambazo hazitumiki katika mavazi na mapambo:

Zaka sio wajibu katika vitu hivyo isipokuwa tu vikifikia kiwango cha kisheria, na vikazungukiwa na mwaka mzima wa mwezi muandamo ambao hisabu yake ni  siku 354.

Kiwango cha zaka katika Dhahabu na Fedha ni kama ifuatavyo: 

Dhahabu ni takriban gramu 85, na Fedha gramu 595. 

Ikiwa Muislamu anamiliki kiwango hiki na kikazungukiwa na mwaka, atatoa zaka ya asilimia 2.5%.

 1. Hela na sarafu kwa aina zake zote, sawa ziwe ziko mkononi mwake au zimehifadhiwa benki.

Utoaji wa zaka yake: Kiwango cha hela na sarafu kinahesabiwa kwa thamani ya dhahabu. Kama hela au sarafu inalingana na kiwango cha dhahabu au kinazidi kiwango cha dhahabu ambacho ni takriban gramu 85 katika wakati wa kulazimika kutoa zaka, na ikawa umepita mwaka wa mwezi muandamo huku hela hiyo ikiwa bado ni mali yake, basi atatoa zaka ya asilimia 2.5%.

Mfano: Thamani ya dhahabu inabadilika. Kama tukichukulia  kwamba thamani ya dhahabu wakati wa kulazimika kutoa zaka ni sawa na Dola 25, basi kiwango cha hela kitakuwa kama ifuatavyo: 

25 (Thamani ya gramu ya dhahabu ambayo inabadilika badilika) x85 (idadi ya gramu ambayo haibadiliki) = Dola 2,125. Hicho ndicho kiwango cha hela.

 1. Bidhaa za biashara:

Maana yake: Ni kila kitu kilicho andaliwa kwa ajili ya biashara, ikiwa ni pamoja na mali isiyo hamishika kama vile viwanja, nyumba na majengo mengine, au bidhaa kama vile vyakula na bidhaa nyingine zitumiwazo.

Namna ya kutoa zaka yake: Mtu anatakiwa kuhesabu thamani ya vitu vyote alivyoviweka kwa ajili ya biashara, pale utakapopita mwaka mzima. Tathmini itakuwa kwa bei ya soko kwa siku hiyo anayotaka kutoa zaka.  Thamani ya bidhaa hizo ikifika kiwango cha zaka ya hela, ataitolea zaka ya robo ya asilimia kumi (2.5%).

 1. Mazao, matunda na nafaka zitokazo ardhini:

Allah  amesema kuwa: «Enyi mlioamini, toeni katika vile vizuri mlivyo vichuma na katika vile tulivyo kutoleeni ardhini». (Sura Albaqara, aya 267).

Zaka ni wajibu katika aina maalumu za mazao, na sio katika mazao yote, kwa sharti la kufikia kiwango maalumu cha kisheria.

Na kunakuwa na tofauti kati ya mazao yanayolimwa kwa kutumia mvua na yanayolimwa kwa kutumia gharama. Imeangaliwa katika kiwango cha lazima cha kutoa zaka kwa kuangalia hali za watu. 

Masharti ya kulazimika kwa zaka ya mazao na matunda:

 1. Mazao yafikie kiwango:

Mtume, swallalahu alayhi wasalam, ameainisha kiwango ambacho zaka inakuwa wajibu katika kiwango hicho, na haiwi wajibu katika kiwango ambacho ni  chini ya hapo. Amesema: «Chini ya wakia tano za tende hakuna zaka». (Bukhari, Hadithi Na. 1447. Muslim, Hadithi Na. 979).

Hicho ni kipimo cha ujazo. Lakini kwa kipimo cha uzito, kwa zao la ngano na mchele inakisiwa kuwa kati ya kilogramu 580 na kilogramu 600.  Chini ya kiwango hicho hakuna zaka.

 1. Mazao yawe katika yale yanayo takiwa kutolewa zaka: 

Zaka sio wajibu isipokuwa tu katika mazao ambayo yanaweza kuwa chakula ambacho, kwa kawaida, kinamfanya mwanadamu aishi, na ambacho inawezekana kukihifadhi kwa muda mrefu bila ya kuharibika, kama vile ngano, shairi, zabibu, tende, mchele na mahindi. Ama jamii ya matunda na mbogamboga ambazo haiwezekani kuzihifadhi kwa muda mrefu na kuzitegemea kama chakula, zaka sio wajibu katika mazao hayo. Mfano ni kama tikitimaji, komamanga, saladi, viazi, karoti, karanga, korosho na mfano wake.

 1. Kufika kwa muda wake wa kuvunwa:

Zaka inakuwa wajibu katika mazao na matunda yatakapokuwa yamevunwa, na wala hayafungamanishwi na kupita kwa mwaka. Kama mazao yanavunwa mara mbili kwa mwaka, zaka itakuwa wajibu katika kila mavuno (atatoa zaka mara mbili). Kama mtu kayatolea zaka mazao yake, kisha akayahifadhi kwa miaka kadhaa, hakuna zaka katika miaka hiyo. 

 1. Mifugo

Makusudio ya mifugo ni wanyama wa kufuga ambao  binadamu anafaidika nao, hasa hasa ni: Ngamia, Ng`ombe, Mbuzi na Kondoo tu.

Allah amejisifu kwa waja wake kwamba amewapa neema ya kuwaumbia wanyama hao ili wanadamu wale nyama zao, wavae nguo zitokanazo na manyoya yao na kuwabebea mizigo yao katika kusafiri. Allah amesema kuwa: «Na amekuumbieni wanyama wa kufuga ambao wana (kupeni vazi linalokupeni vuguvugu la) joto na manufaa mengine, na wengine mnakula. Na wanakupeni mandhari nzuri (ya kukufurahisheni) mnapowapeleka malishoni asubuhi na mnapowarudisha jioni. Na wanabeba mizigo yenu na kuifikisha katika miji ambayo msingeweza kuifikia isipokuwa kwa tabu sana. Hakika, Mola wenu ni Mpole sana na Mwenye rehema». (Sura An-nahli, aya 5-7).

Masharti muhimu ya zaka ya mifugo

 1. Wanyama wafikie kiwango cha kisheria; kwa sababu  zaka sio wajibu isipokuwa kwa matajiri tu. Ama wenye kumiliki idadi ndogo ya wanyama kwa mahitaji yao binafsi, hakuna zaka katika wanyama hao. Kiwango cha ngamia ni watano, mbuzi na kondoo ni arubaini na ng`ombe ni thalathini. Chini ya kiwango hicho hakuna zaka.
 2. Mifugo iwe imefika mwaka kamili wa mwezi muandamo ikiwa kwa mmiliki kwake.
 3. Wanyama wawe wanakwenda malishoni. Hawa ni wanyama ambao wanakula majani machungani, na wala mfugaji wake habebi mzigo wa gharama za chakula cha mifugo yake kipindi kikubwa cha mwaka.
 4. Wasiwe wanafanyishwa kazi. Wafanywishao kazi  ni wanyama ambao mmiliki wake anawatumia katika kulima au kubebea mizigo na bidhaa. Hakuna zaka katika wanyama hao.

Allah amewajibisha zaka katika ngamia, n’gombe, mbuzi na kondoo iwapo wanachunga na kula majani na mmiliki wake haingii gharama ya kuwalisha.

Mwongozo Mwepesi wa Muislam

Mtandao wa Mwongozo Mwepesi wa Muislam ni kitabu cha Mtandaoni cha kitabu asili ‘Mwongozo Mwepesi wa Muislam’ ambacho ni moja ya mradi wa Kampuni ya Mwongozo wa Kisasa na kimetolewa katika Lugha Zaidi ya 15 na maudhui yake yameambatana na ujuzi mkubwa wa kimtandao katika kufikisha.

Modern Guide