You are here

Neema kubwa zaidi ulimwenguni

quran and islamic books

Allah amempa mwanadamu neema ambazo hazihesabiki. Kila mmoja miongoni mwetu bado yungali akiishi katika neema za Allah na fadhila zake. Yeye aliyetakasika ndiye aliyetupa neema ya kusikia na kuona wakati ambapo watu wengi wamenyimwa neema hizo. Pia ametupa neema ya akili, afya, mali na familia. Bali pia ametufanya tuutawale ulimwengu wote; kwa jua lake, mbingu yake, ardhi yake na viumbe vyake. «Na mkizihesabu neema za Allah hamtozidhibiti» (Sura Annahli, aya 18).

Lakini neema hizi zote kikomo chake ni pale uhai unapofika tamati. Ama neema pekee ambayo inatoa matunda mema na utulivu duniani, na athari yake kuendelea mpaka Akhera ni neema na muongozo wa Uislamu. Hiyo ni neema kubwa sana aliyoitoa Allah kwa waja wake.

Na kwa sababu hii, Allah ameinasibisha kwake neema hii ili kuitukuza na kuitofautisha na neema nyingine. Allah amesema kuwa: «…leo nimekukamilishieni dini yenu, na nimetimiza kwenu neema yangu, na nimeridhia kwenu Uislamu iwe dini» (Sura Almaida , aya 3).

Uislam ni neema kubwa sana iliyoje aliyoineemesha Allah kwa mwanadamu pale anapomtoa katika giza na kumuweka kwenye nuru, na kumuongoza kwenye dini ya haki ambayo ameiridhia kwake, ili afikie lengo na jukumu la kumuabudu Allah ambalo ameumbwa kwa ajili yake! akitekeleza hilo, anapata mema ya duniani na malipo mazuri ya Akhera!

Pia Uislam ni neema kubwa sana iliyoje aliyoitoa Allah kwetu pindi anapotuchagua na kututeua ili tuwe miongoni mwa umma bora uliodhihirishwa kwa wanadamu ili tubebe neno la Laa ilaaha illallah ambalo Allah amewatuma kwalo Mitume wote, Allah awafikishie rehema na amani.

Wakati baadhi ya watu wajinga walipodhani kuwa fadhila zinarudi kwao katika kuingia kwao katika Uislamu, na kwa hilo wakawa wanamsimanga Mtume, swallalahu alayhi wasalam, Allah  aliwatanabahisha kwamba masimango na fadhila zote zinarudi kwa Allah kwa kuwarahisishia kufuata muongozo wa dini hii. Allah  amesema kuwa: «wanakusimanga kwamba wamesilimu.Sema (uwaambie kuwa): Msinisimange kwa Uislamu wenu. Lakini Allah  anakusimangeni kwamba amekuongozeni kwenye imani, ikiwa nyinyi ni wakweli» (Sura Alhujurat , aya 17).

Neema za Allah ni nyingi. Pamoja na haya, neema pekee ambayo Allah ametusimanga kwayo ni neema ya Uislamu na kupata muongozo wa kumuabudu na kumpwekesha.

Lakini neema hii inahitaji kushukuriwa ili idumu na iimarike, kama Allah alivyosema kuwa: "..kwa yakini kabisa, mkishukuru nitakuongezeeni". (Sura Ibrahim , aya 7).

Mwongozo Mwepesi wa Muislam

Mtandao wa Mwongozo Mwepesi wa Muislam ni kitabu cha Mtandaoni cha kitabu asili ‘Mwongozo Mwepesi wa Muislam’ ambacho ni moja ya mradi wa Kampuni ya Mwongozo wa Kisasa na kimetolewa katika Lugha Zaidi ya 15 na maudhui yake yameambatana na ujuzi mkubwa wa kimtandao katika kufikisha.

الدليل المعاصر