You are here

Kumuamini Allah

Kusujudu ni miongoni mwa dalili kubwa za unyenyekevu kwa Muumba.

Maana ya Kumuamini Allah:

Ni imani thabiti ya kuamini kuwepo kwa Allah alietukuka na kukubali kuwa yeye ndiye Mola, ndiye muabudiwa, pia kuamini majina na sifa zake.

Tutayazungumzia mambo haya manne kwa ufafanuzi kama ifuatavyo:

  1. Kuamini Uwepo wa Allah subhanahu wa’taala

Kukubali kuwepo kwa Allah Mtukufu ni jambo la kimaumbile kwa mwanadamu lisiliohitaji kujikalifisha katika kulitolea ushahidi. Na kwa sababu hii, watu wengi sana wanakiri kuwepo kwa Allah pamoja na kutafautiana dini zao na madhehebu yao.

Sisi tunahisi kutoka ndani ya nyoyo zetu kwamba Allah yupo; tunamkimbilia katika shida na majanga kwa maumbile yetu yanayoamini na silka ya kuamini dini ambayo Allah ameiweka katika nafsi ya kila mwanadamu, japokuwa baadhi ya watu wanajaribu kuififiliza na kuipuuza.

Nasi tunasikia na tunaona katika majibu ya wanao omba dua, wapewayo waombaji na wenye matatizo kutatuliwa shida zao tunasikia na kuona mambo ambayo yanatoa ushahidi wa yakini juu ya kuwepo kwa Allah. .

Ushahidi wa kuwepo kwa Allah uko wazi zaidi usiohitaji kutajwa na kuhesabiwa. Miongoni mwa ushahidi huo ni huu:

  • Ni jambo linalojulikana kwa kila mtu kwamba tukio lolote halina budi kuwa na aliyelitenda. Viumbe vyote hivi vingi na ambavyo tunaviona kila wakati ni lazima vina muumba aliyevifanya viwepo, naye ni Allah. Ilivyo ni kwamba haiwezekani kuwa vimeumbwa bila ya muumba aliyeviumba. Kama ambavyo pia haiwezekani kuwa vimejiumba vyenyewe, kwa sababu kitu hakijiumbi chenyewe, kama Allah alivyosema kuwa: «Au wameumbwa bila ya jambo au wao ndio waumbaji?». (Sura Attuur, aya 35). Maana ya aya ni kwamba wao hawakuumbwa bila ya muumbaji, wala wao pia hawakujiumba wenyewe. Hivyo, inalazimika kuwa muumba wao ni Allah.
  • Mfumo wa huu ulimwengu kwa mbingu zake, nyota zake na miti yake unatoa ushahidi usiokuwa na shaka kwamba huu ulimwengu una muumba mmoja, naye ni Allah. «Utengeneaji wa Allah ambaye amekitengeneza vizuri kila kitu». (Sura Annamli, aya 88).

Hizi sayari na nyota, kwa mfano, zinatembea katika mpangilio madhubuti usiotetereka. Kila sayari inatembea katika njia ambayo haiikeuki na haiipitilizi.

Allah anasema kuwa: Si jua linalotakiwa kuuwahi mwezi na si usiku unaoutangulia mchana. Na kila kimoja katika njia kinatembea». (Sura Yasin, aya 40).

  1. Kuamini kuwa Allah ni mola:

Maana ya kuamini kuwa Allah ni Mola:

Ni kukubali na kuamini kuliko thabiti kwamba Allah ni Mlezi wa kila kitu, mmiliki wake, muumba wake, anayekipa riziki na kwamba yeye ndiye mletaji uhai, mletaji kifo, mletaji manufaa, mletaji madhara, ambaye mambo yote ni yake yeye, naye anaweza kila jambo, hana mshirika katika hayo.

Kwa hiyo, imani hiyo ni kuamini kuwaa Allah ni pekee katika matendo yake, na hiyo ni kwa mtu kuwa na itikadi kwamba:

  • Allah peke yake ndiye muumba wa vyote vilivyopo ulimwenguni, na hakuna muumba mwengine, kama Allah alivyosema kuwa: «Allah ndiye muumba wa kila kitu». (Sura Azzumar, aya 62).
    Ama utengenezaji wa mwanadamu ni wa kugeuza kutoka katika sifa fulani kwenda kwenye sifa nyingine au kukusanya na kuunda, na mfano wa hayo, na sio uumbaji wa kweli na sio kuumba kutoka kisichokuwepo, na sio kuleta uhai baada ya mauti.
  • Na yeye ndiye mwenye kuvipa riziki viumbe vyote, na hakuna mtoaji riziki asiyekuwa yeye, kama Allah anavyosema kuwa: «Na hakuna kitu mbaacho katika ardhi isipokuwa kwamba ni juu ya Allah riziki yake».  (Sura Huud, aya 6).
  • Na yeye ndiye mmiliki wa kila kitu, na hakuna mmiliki wa kweli asiyekuwa yeye, ambapo Allah anasema kuwa: «Ni wa Allah tu umiliki wa mbingu na ardhi na vilivyomo ndani yao». (Sura Almaida, aya 120).
  • Na kwamba yeye ndiye mwendeshaji wa kila jambo, na hakuna mwendeshaji ila Allah pekee, kama Allah alivyosema kuwa: «anatengeneza mambo kutoka mbinguni mpaka ardhini». (Sura Assajda, aya 5).Ama uendeshaji wa mwanadamu kwa mambo yake, maisha yake na kuyapangilia umefungika na unahusika tu na mambo yaliyopo ndani ya uwezo wake na ambayo anayamiliki na kuyaweza. Uendeshaji huo unaweza kufanikiwa na unaweza kufeli. Lakini uendeshaji wa Allah Mtukufu ni mpana, hakuna kinachoweza kujitoa, na ni wenye kufanyika; hakuna kinachoweza kuuzuia au kuukwamisha, kama Allah Mtukufu alivyosema kuwa: «Ee! Ni kwake yeye tu kuumba na kuamrisha. Ametukuka Allah Mola wa walimwengu». (Sura Al-aaraf, aya 54). 

Makafiri wa Kiarabu wakati wa Mtume swallalahu alayhi wasalam walikuwa wakikiri kwamba Allah ndie mola mlezi wa ulimwengu:

Makafiri wakati wa Mtume wa Allah swallalahu alayhi wasalam, walikiri kwamba Allah ndiye Muumba, Mmiliki na Muendeshaji mambo. Hilo pekee halikuwaingiza katika Uislamu, kama Allah alivyosema kuwa: «Na kwa yakini kabisa, ukiwauliza: Ni nani aliyeumba mbingu na ardhi? Bila ya shaka yoyote, watasema: Ni Allah». (Sura Luqman, aya 25).

Kwa sababu aliyekiri kwamba Allah ni Mola wa walimwengu, kwa maana ya kuwa ni Muumba wao, Mmiliki wao na Mlezi wao kwa neema zake inamlazimu kumkusudia yeye peke yake kwa ibada na kumfanyia ibada hizo yeye tu asiyekuwa na mshirika.

Ni vipi iingie akilini kwamba mtu anakiri kwamba Allah ni Muumba wa kila kitu, Muendeshaji wa ulimwengu, Mletaji uhai na Mletaji mauti halafu mtu huyo anafanya jambo katika aina za ibada kumfanyia asiyekuwa Allah? Hii ndio dhuluma mbaya sana na dhambi kubwa sana. Kwa sababu hii, Luqman alimwambia mwanae akimpa nasaha na maelekezo kwamba: «Ewe kijana wangu, usimshirikishe Allah Kwa yakini, ushirika ni dhuluma kubwa». (Sura Luqman, aya 13).

Na Mtume, swallalahu alayhi wasalam alipoulizwa kwamba: Ni dhambi gani kubwa sana mbele ya Allah? Alisema: «Ni wewe kumfanyia Allah mshirika na ilhali yeye ndiye aliyekuumba». (Bukhari hadithi Na. 4207. Muslim Hadithi Na. 86).

Kuamini kuwa Allah ni Mola kunazipa nyoyo utulivu:

Mja akijua kwa yakini kwamba haiwezekani kwa kiumbe yeyote kuyaepuka aliyoyapanga Allah kwa kuwa Allah ndiye Mmiliki wao anayefanya atakavyo kwa mujibu wa hekima na busara zake, naye ndiye Muumba wao wote na kwamba kila asiyekuwa Allah basi ameumbwa au kimeumbwa hivyo kinamhitaji Muumba wake na kwamba mambo yote yako mkononi mwa Allah; hakuna Muumba ila yeye tu, hakuna mtoaji riziki ila yeye tu, hakuna muendeshaji ulimwengu ila yeye tu, hakuna chembechembe yoyote inayotikisika ila kwa idhini yake na hakuna inayotulizana ila kwa amri yake tu, hilo linaacha katika moyo wake uhusiano na Allah pekee, kumuomba, kumhitaji, kumtegemea katika mambo yote ya maisha yake, kupambana na kuwa na bidii katika harakati za maisha kwa utulivu, ari na bidii, kwa sababu  mwanadamu ametekeleza sababu ya kutafuta anayoyataka katika mambo ya maisha yake na amemuomba Allah ili amtekelezee matakwa yake, basi amekwisha tekeleza wajibu wake. Hapo, nafsi yake inatulia na kuacha kuyakodolea macho mambo yaliyoko kwa watu wengine. Mambo yote kwa ukweli yako kwa Allah,anaumba atakayo na anachagua.

Mwongozo Mwepesi wa Muislam

Mtandao wa Mwongozo Mwepesi wa Muislam ni kitabu cha Mtandaoni cha kitabu asili ‘Mwongozo Mwepesi wa Muislam’ ambacho ni moja ya mradi wa Kampuni ya Mwongozo wa Kisasa na kimetolewa katika Lugha Zaidi ya 15 na maudhui yake yameambatana na ujuzi mkubwa wa kimtandao katika kufikisha.

الدليل المعاصر