You are here

Nafasi ya familia katika Uislamu

Namna Uislamu unavyoijali familia unaonekana wazi katika mambo yafuatayo:

  1. Uislamu umetilia mkazo sana suala la kuoa na kuanzisha familia. Umelifanya suala hilo kuwa ibada kubwa sana na ni katika mwenendo wa Mitume. Amesema Mtume, swallalahu alayhi wasalam, kuwa: «Lakini mimi ninafunga swaumu na ninafungua. Ninaswali usiku na ninalala,  na ninaoa wanawake. Kwa hiyo, mwenye kupinga mwenendo wangu (huu) sio mwenzangu». (Bukhariy, Hadithi Na. 4776. Muslim, Hadithi na. 1401)
  • Qur`ani inahesabu kwamba yale mambo ambayo Allah ameyaumba kwa mume na mkewe, ikiwa ni pamoja na utulivu, mapenzi, huruma na kuliwazika ni miongoni mwa neema, alama na miujiza mikubwa sana. Amesema Allah Mtukufu kuwa: «Na ni miongoni mwa alama zake kwamba amekuumbieni wake watokanao na nyinyi ili mpumzike kwao, na akajaalia baina yenu mapenzi na huruma».(Arruum, aya 21)
  • Uislamu umeamrisha suala la ndoa lifanywe jepesi na kumsaidia anayetaka kuoa ili apate hifadhi. Amesema Mtume, swallalahu alayhi wasalam, kuwa: «Watu wa aina tatu ni haki kwa Allah  kuwasaidia watu hao» na akataja miongoni mwa watu watatu hao kuwa ni, «..na muoaji ambaye anakusudia kujihifadhi». (Tirmidhiy, Hadithi Na. 1655).
  • Uislamu umewaamrisha vijana ambao wako katika kilele cha ujana wao na nguvu zao kwamba waoe, kwa sababu katika kuoa kuna utulivu na suluhisho la kisheria la  kukidhi nguvu za matamanio yao. 

Uislamu unaichukulia ndoa na kujenga familia kuwa ni miongoni mwenendo wa Mitume, na umeamrisha kulifanya jambo hilo kuwa jepesi na kuwasaidia vijana walifanye.

  1. Uislamu umempa heshima kamili kila mtu katika familia, sawa awe mwanamke au mwanaume:

Uislamu umembebesha baba na mama majukumu makubwa ya kulea watoto wao. Imenukuliwa kwa Abdallah Bin Omar, Allah amuwiye radhi, akisema kuwa  alimsikia Mtume wa Allah akisema kwamba: «Kila mmoja wenu ni mchungaji, na ataulizwa juu ya kile alichokichunga.  Imamu ni mchungaji na ataulizwa juu ya kile alichokichunga. Na mwanaume ni mchungaji katika familia yake, naye ataulizwa juu ya kile alichokichunga. Na mwanamke ni mchungaji katika nyumba ya mume wake, naye ataulizwa juu ya kile alichokichunga. Na mtumishi ni mchungaji katika mali ya mwajiri  wake, naye ataulizwa juu ya kile alichokichunga».(Bukhariy, Hadithi Na. 853. Muslim, Hadithi Na. 1829)

  1. Uislamu umefaradhisha kwa Muislamu kuimarisha udugu. Maana ya kuimarisha udugu ni Muislamu kuwa na mawasiliano mazuri na ndugu zake wa upande wa baba na mama na kuwafanyia mambo ambayo ni mazuri: 

Kama vile kaka na wadogo zake, dada zake, ami zake na watoto wao, shangazi zake, wajomba zake, mama zake wakubwa na wadogo na watoto wao. Uislamu umelihesabu jambo hilo kuwa ni miongoni mwa ibada kubwa sana. Pia Uislamu umekataza kuwakatia udugu au kuwafanyia mambo mabaya, na umelihesabu jambo hilo kuwa ni miongoni mwa madhambi makubwa sana. Mtume, swallalahu alayhi wasalam, amesema kuwa: «Haingii peponi mtu mwenye kukata udugu».(Bukhariy, Hadithi Na. 5638. Muslim, Hadithi Na. 2556)

  1. Uislamu umehimiza kupanda mbegu ya msingi wa kuwa na adabu na heshima kwa wazazi, kuwahudumia na kuwatii mpaka kufa:

Mtoto wa kike au wa kiume hata kama ni mtu mkubwa kiasi gani, ni wajibu kwao kuwatii wazazi wao na kuwafanyia mambo mazuri. Allah amelikutanisha pamoja jambo hilo na kuabudiwa kwake. Pia amekataza kuwakosea adabu kwa vitendo au maneno, hata kama hilo litafanyika kwa kutamka wazi neno moja au sauti inayo onesha kukerwa nao. Allah Mtukufu amesema kuwa: «Na Mola wako amehukumu kwamba msiabudu (chochote) isipokuwa yeye tu na kuwanfanyia wazazi mambo mazuri. Kama mmoja wao atafikia uzee au wote wawili ukiwa nao, basi usiwaambie hata Ah!  wala usiwafokee, na sema nao kwa maneno mazuri».(Al-israa,aya 23)

  1. Kufanya uadilifu kwa watoto

Uislamu umeamrisha kulinda haki za watoto wakike na wakiume katika matunzo na mambo ya dhahiri. Mtume, swallalahu alayhi wasalam, amesema kuwa: «Mcheni Allah na fanyeni uadilifu kwa watoto wenu». (Bukhariy 2650).

Mwongozo Mwepesi wa Muislam

Mtandao wa Mwongozo Mwepesi wa Muislam ni kitabu cha Mtandaoni cha kitabu asili ‘Mwongozo Mwepesi wa Muislam’ ambacho ni moja ya mradi wa Kampuni ya Mwongozo wa Kisasa na kimetolewa katika Lugha Zaidi ya 15 na maudhui yake yameambatana na ujuzi mkubwa wa kimtandao katika kufikisha.

الدليل المعاصر