You are here

Vyanzo vya Sheria katika Uislamu

Waislamu katika kujua sheria za Kiislamu wanategemea misingi na hoja kuu ambazo wanachukua humo elimu ya kujua matukio kwamba ni halali au ni haramu.    

Hoja kuu za sheria ni kama ifuatavyo:

 1. Qur’ani Tukufu: 

Hiki ni kitabu cha Allah kilicho teremshwa kwa waja wake, ni ufafanuzi na ni kitenganishi kati ya haki na batili. Kina kinga ya kutobadilishwa na kutopotoshwa. Allah anapoamrisha au anapokataza katika kitabu chake, ni wajibu kwa Waislamu wote kutii muktadha wa amri hiyo au makatazo hayo. Allah asemapo kuwa: «Na simamisheni Swala» (Sura Annuur, aya 56), tunajua kwa yakini kuwa Swala ni wajibu. Na Allah asemapo kuwa: «Na msiisogelee Zinaa, kwa kuwa ni jambo chafu na ni njia mbaya» (Sura Al-israi, aya 32), tunajua kwa yakini kuwa Zinaa ni haramu. Kwa kuwa Allah amebeba jukumu la kuilinda Qur’ani isibadilishwe, isizidishwe au kupunguzwa tunachohitaji sisi ni kuhakikisha tu kwamba aya inalenga jambo gani.     

 1. Sunna za Mtume: 

Sunna ni kila jambo sahihi lililohusishwa na Mtume, swallalahu alayhi wasalam, iwe ni kauli zake au vitendo vyake au tabia zake au ukimya wake (kupata taarifa ya jambo lililofanywa na akakaa kimya bila ya kulitolea kauli). Iwapo tutajua kwamba ni sahihi kauli ya Mtume isemayo kuwa: «Hapajumuishwi (katika ndoa) kati ya mwanamke na shangazi yake wala kati ya mwanamke na mama yake mdogo au mkubwa» (Bukhariy, Hadithi Na. 5109), tutafahamu kuwa haifai na wala haiwi sahihi mtu kumuoa mwanamke na akaoa pamoja naye shangazi wa mwanamke huyo au mama yake mkubwa au mdogo.  

Ili kuchukua sheria katika Sunna za Mtume, Sunna inatazamwa katika vipengele viwili:

 • Usahihi wa kuhusishwa hadithi kwa Mtume, swallalahu alayhi wasalam. Wanazuoni wa Kiislamu wamefanya juhudi kubwa na kwa vigezo vya hali ya juu vya umakini na umahiri katika kuzipitia Sunna za Mtume na kuzitenganisha Hadithi sahihi zilizothibiti kwa nukulu za watu madhubuti na kuziweka kando kauli ambazo zinahusishwa na Mtume wakati ambapo sio Sunna zake. Kauli hizo inawezekana zimetokea kwa kukosea au kwa kudhani au kwa sababu ya uongo wa baadhi ya maadui wa Uislamu.
 • Hadithi kuwa na maana inayokusudiwa. Maana inaweza 
  kuwa ubainifu na ya wazi isiyoleta utofauti, na inaweza kuwa na maana zaidi ya moja au isiyofahamika ila tu kwa kuihusisha kwenye Hadithi nyingine.
 1. Ijmaa:

Ijmaa ni wanazuoni wote wa Kiislamu kuafikiana juu ya jambo fulani katika zama zote. Wanazuoni wa Kiislamu wameafikiana katika Sheria nyingi kuu za Kiislamu na hawakutafautiana. Mfano: Idadi ya rakaa za Swala, wakati wa kufunga na kufungua katika swaumu, kiwango cha Zaka ya Dhahabu na Fedha n.k.     

Maswahaba na waliokuja baada yao wanapoafikiana juu ya jambo Fulani inakuwa ushahidi sahihi wa jambo hilo, kwa sababu umma hauwezi kuafikiana juu ya kosa.

 1. Qiyaas (Ulinganishi):

Qiyaas ni kulitolea hukumu jambo ambalo halimo katika Qur’ani na Sunna kwa kutumia hukumu ya jambo jingine lililomo katika Qur’ani na Sunna kwa sababu ya kulingana kwao katika sababu ya hukumu hiyo. Mfano: Tunaposema kuwa ni haramu kuwapiga wazazi, hii ni kwa sababu ya kulinganisha na uharamu wa kuwatolea kauli za kuonesha kukerwa na kuwakaripia. Allah amesema kuwa: «Usiwaambie Ah!, na usiwakemee». (Sura Bani Israil, aya 23). Kwa kuwa Allah amekutaka usiwaudhi, basi uharamu wa kuwapiga upo wazi zaidi kwa sababu mambo yote mawili yanakutana katika sababu ambayo ni kuudhi. Mlango huu ni nyeti, na unawahusu wanazuoni makini. Kwa kutumia Qiyaas zinajulikana hukumu na sheria za masuala yanayotokea wakati wa huu. 

Kwa nini Wanazuoni wanatafautiana pamoja na kukubaliana kwao juu ya vyanzo vya Sheria?

Ili kujua hilo, ni wajibu kutambua mambo yafuatayo:

 1. Wanazuoni wote wanakubaliana juu ya masuala ya imani, misingi ya sheria, nguzo za Uislamu na misingi yake mikubwa. Tafauti zimehusika tu katika baadhi ya ufafanuzi wa sheria na utekelezaji wake.   

Ama kanuni kuu na misingi ya sheria, wanazuoni wameafikiana kwa fadhila za Allah ambaye ameineemesha sheria hii ambayo ni hitimisho la sheria za mbinguni na ambay Allah amedhamini kuilinda mpaka mwisho wa dunia hii.  

 1. Kutafautiana katika mambo uchambuzina ufafanuzi ni jambo la kawaida. Hakuna sheria ya mbinguni au iliyowekwa na wanadamu inayoweza kuliepuka hilo. Pia hakuna taaluma inayoweza kuliepuka hilo. Wanasheria wanatafautiana katika kuifasiri sheria na kuifafanua, na mahakama zinatafautiana katika kuitekeleza.

Wanahistoria wanatafautiana katika simulizi za historia na matukio yake. Madaktari, wahandisi na wanasanifu wanatafautiana katika jambo moja katika kulitazama na kulifafanua.
Kutafautiana katika mambo ya yasiyo ya asili katika dini ni jambo la kawaida ambalo maisha ya kitaaluma na kiutendaji yanalihitaji.

 1. Allah amemsamehe mwenye kuitafuta haki kwa kutumia njia sahihi na akakosea kuifikia. Mtume, swallalahu alayhi wasalam, amempa habari njema mwenye kuitafuta kwa kutumia njia sahihi kwamba, hatakosa thawabu katika hali zote mbili.  

Akiipatia haki atapata thawabu mara mbili, na akikosea huku akiwa amefanya bidii ya kufuata njia sahihi, atapata thawabu mara moja. Mtume, Allah amfikishie rehema na amani, amesema kuwa: «Akihukumu hakimu, akajitahidi halafu akapatia atapata malipo mara mbili. Na akihukumu, akajitahidi halafu akakosea atapata malipo mamoja». (Bukhariy, Hadithi Na. 7352). 

Allah amehadithia kisa cha Mtume Daudi na Mtume Suleiman, Allah awafikishie amani, pale walipopewa kesi ili watoe hukumu. Wote walijitahidi, na Mtume Suleiman akahukumu sawa lakini Mtume Daudi hakuwezeshwa kuhukumu kama hivyo. Allah amesimulia kisa chao na kuthibitisha usahihi wa hukumu ya Suleiman na makosa ya Daudi. Pamoja na hayo, Allah amewasifia wote.  Amesema kuwa: «Tukampa fahamu ya hukumu hiyo Suleiman, na wote tumewapa hukumu na elimu». (Sura Al-anbiyaa, aya 79).

 1. Wanazuoni wote wanaokubalika pamoja na Maimamu wa Madhehebu Manne wanategemea Qur’ani na Sunna, na hawaweki mbele maoni binafsi au upinzani. Kutofautiana kwao hakutokani na upenzi binafsi au kutetea maslahi binafsi. Kutofautiana kwao kulitokana na misingi ya kitaaluma inayokubalika katika kuiendea haki. Inawezekana Hadithi ikamfikia mwanachuoni mmoja na isimfikie mwenzake, au inawezekana mtazamo wa kitaaluma katika kutafakari hoja za Qur’ani na Sunna ukatafautiana, n.k. 
 2. Wanazuoni Wanne miongoni mwa wanazuoni na wanasheria wakubwa wa Kiislamu wamekuwa mashuhuri na watu wamekubaliana juu ya uongozi wao katika dini na elimu. Wana kiwango cha juu cha elimu, ufahamu wa sheria na dini. Wanafunzi wao ni wengi ambao wameeneza elimu yao na kuwafundisha sehemu mbali mbali duniani, na kwa sababu hiyo yamepatikana kwetu Madhehebu Manne yaliyo enea katika nchi za Waislamu yakihusishwa nao. 

       Wanazuoni hao ni kama ifuatavyo:

 • Imamu Abuhanifa. Jina lake ni Nouman Bin Thabit. Aliishi Iraq na kufariki mwaka 150 Hijiriya (768 Miladiya). Madhehebu ya Hanafi yanahusishwa na yeye. 
 • Imam Malik Bin Anas Al-asbahiy, Imamu wa mji wa Madina. Alifariki mwaka 179 Hijiriya (796 Miladiya). Madhehebu ya Maliki yanahusishwa na yeye.
 • Imam Shaafii. Jina lake ni Muhammad Bin Idrisa. Aliishi Makka, Madina, Iraq na Misri. Alifariki mwaka 204 Hijiriya (820 Miladiya). Madhehebu ya Shaafii yanahusishwa na yeye. 
 • Imam Ahmad Bin Hanbal. Umri wake mwingi aliishi Iraq. Alifariki mwaka 241 Hijiriya (856 Miladiya). Madhehebu ya Hanbal yanahusishwa na yeye.

Baina ya Maimamu Wanne na baina ya wanafunzi wao kulikuwepo kusifiana na aina mbali mbali za kupeana taaluma. Wote walikuwa na bidii ya kuifuata haki, na kila mmoja hakuona shida kukubaliana na fulani katika suala fulani na kukubaliana na mwengine katika suala jingine kwa lengo la kuifuata haki na hoja. Kwa sababu hii, tunakuta kuwa baadhi yao wamesoma kwa wengine. Imamu Ahmad amesoma kwa Imam Shaafii, na Imam Shaafii amesoma kwa Imam Malik. Baina ya Imam Malik na wanafunzi wa Imam Abuhanifa kulikuwepo na vikao na darasa za kitaaluma.    

Imethibiti kunukuliwa kwa maimamu wote wanne kauli yao isemayo kuwa: «Hadithi ikiwa sahihi, hayo ndio madhehebu yangu». Lengo lao la kwanza ni kueneza elimu na kuwaondolea watu ujinga. Tunamuomba Allah awarehemu rehema pana. 

Ni upi wajibu wa Muislamu katika tofauti za wanachuoni katika Sheria?

Wajibu wa Muislamu ni kufanya juhudi katika kuifuata haki na kuiendea.

 • Muislamu akiwa ni miongoni mwa wanafunzi wa sheria wazamivu katika kudurusu na kutafiti hoja, inamlazimu kufuata yale ambayo juhudi zake zimemfikisha katika kuzifahamu hoja kwa mujibu wa kanuni za taaluma ya sheria za Kiislamu (Fiq-hi). Ni haramu kwake kumshabikia shekhe wake au madhehebu yake iwapo itamdhihirikia kwamba usahihi upo kwa shekhe mwengine.
 • Ama kama Muislamu ni miongoni mwa Waislamu wa kawaida na sio mtafiti wa hoja, inamlazimu kumfuata shekhe muaminifu zaidi kwake katika dini na elimu yake. Kwa kufanya hivyo, atakuwa ametimiza wajibu wake na atakuwa amefuata kauli ya Allah isemayo kuwa: «Waulizeni wenye utambuzi ikiwa nyinyi hamjui». (Sura Al-anbiyaa, aya 7).

Akishajua kauli madhubuti au akishamuuliza mwanachuoni madhubuti kuhusu suala fulani, halazimiki baada ya hapo kumuuliza yeyote. Endapo atajua kuwa kuna kauli inayopingana na hiyo, ni wajibu wake kufuata kauli ambayo anadhani kuwa iko karibu sana ya haki na usahihi, kama vile mgonjwa anavyofanya pale madaktari wanapotafautiana juu ya wasifu wa matibabu yake. 

Ni wajibu wake kuacha kumkejeli au kumkemea Muislamu mwenzake ikiwa atatafautiana naye katika mtazamo, madamu mwenzake amefuata madhehebu ya kisheria au amemfuata Imamu anayekubalika au iwapo mwenzake huyo ni miongoni mwa wanataaluma wa sheria ya dini wenye uwezo wa kutafiti katika masuala ya sheria. Maswahaba na Wema Waliotangulia walikuwa wakitafautiana katika masuala ya sheria huku wakiwa wanapendana, wakiwa ndugu na kujadiliana bila ya kukejeliana.    

Mwongozo Mwepesi wa Muislam

Mtandao wa Mwongozo Mwepesi wa Muislam ni kitabu cha Mtandaoni cha kitabu asili ‘Mwongozo Mwepesi wa Muislam’ ambacho ni moja ya mradi wa Kampuni ya Mwongozo wa Kisasa na kimetolewa katika Lugha Zaidi ya 15 na maudhui yake yameambatana na ujuzi mkubwa wa kimtandao katika kufikisha.

الدليل المعاصر