You are here

Maadili ambayo Uislamu umesisitiza yawepo katika miamala ya kifedha

Kama ambavyo Uislamu umeweka wazi sheria za miamala ya kifedha, umeweka mkazo maadili na taratibu kadha za kufuatwa na watu wanaofanya miamala hiyo. Miongoni mwa taratibu na maadili hayo ni haya:

Uaminifu

Uaminifu katika kufanya miamala ya kibiashara na watu, sawa wawe Waislamu au sio Waislamu ni miongoni mwa maadili muhimu sana kwa Muislamu anayefuata sheria za Allah. Msisitizo huu unajitokeza wazi katika maelezo yafuatayo: 

  • Amesema Allah Mtukufu kuwa: «Hakika, Allah anakuamrisheni kurejesha amana kwa wenyewe».(Annisaa, aya 58)
  • Mtume, swallalahu alayhi wasalam, ameuhisabu ukosekanaji wa uaminifu kwamba ni miongoni mwa alama za unafiki, pale aliposema kuwa: «Alama za mnafiki ni tatu: Akizungumza anasema uongo, na akitoa ahadi hatekelezi, na akiaminiwa anavunja uaminifu». (Bukhariy, Hadithi Na. 33. Muslim, Hadithi Na. 59)
  • Uaminifu ni miongoni mwa sifa kubwa sana za waumini. Allah Mtukufu amesema kuwa: «Kwa yakini, wamefaulu waumini..».. mpaka akasema: «…na ambao amana zao na ahadi zao wanazichunga».(Almuuminuun, aya 1-8).  Kwa sababu hii, Mtume amekataa uwepo wa imani kwa mtu ambaye hana uaminifu, na kusema kuwa: «Imani haipo kwa mtu asiyekuwa na uaminifu».(Ahmad, Hadithi Na.12567)
  • Mtume, swallalahu alayhi wasalam, alipokuwa Makka kabla ya kupewa utume alipewa jina la umaarufu la «Mkweli Muaminifu», kwa sababu yeye alikuwa nembo ya uaminifu katika mahusiano yake na miamala yake na watu.

Ukweli

Ukweli na uwazi ni sifa muhimu sana ambazo Uislamu unazihimiza:

  • Mtume, swallalahu alayhi wasalam, amewaelezea muuzaji na mnunuzi kwamba: «Wakiwa wakweli na wawazi, watabarikiwa katika biashara yao. Na wakiwa wasiri na waongo, baraka ya biashara yao inaondolewa». (Bukhariy, Hadithi Na. 1973. Muslim, Hadithi Na. 1532)
  • Mtume, swallalahu alayhi wasalam, amesema kuwa: «Jilazimisheni kusema ukweli, kwa sababu ukweli unasababisha wema, na wema unasababisha kupata pepo. Na mtu haachi kuwa mkweli na kujibidiisha kusema ukweli mpaka aandikwe kwa Allah kwamba yeye ni mkweli».(Muslim, Hadithi Na. 2607)
  • Mtu ambaye ana’apa kwa uongo katika kuisifia biashara yake ili aiuze, Uislamu unamzingatia kwamba amefanya dhambi kubwa katika yale madhambi makubwa sana. Mtume, swallalahu alayhi wasalam, amesema kuwa: «Watu watatu Allah hatawasemesha Siku ya Kiama na hatawatazama na hatawatakasa na watapata adhabu kali» na akataja kuwa miongoni mwa watu hao watatu ni: «..na mwenye kushawishi kuuza bidhaa zake kwa kiapo cha uongo». (Muslim, Hadithi Na. 106) 

Ufanisi na ufanyaji mzuri wa kazi 

Ni wajibu kwa kila Muislamu anayefanya kazi kwamba ukamilifu, ufanisi na uzuri wa kazi  ndio msimamo na maadili yake ambayo hayuko tayari kuyaacha hata kidogo. 

Allah amefaradhisha ufanyaji uzuri katika kila jambo, na akaamrisha lifanyike hilo katika nyanja zote za maisha, hata katika mambo ambayo kwa mtazamo wa haraka haraka inaonekana kuwa haiwezekana kufanya uzuri katika mambo hayo, kama vile kuwinda na kuchinja. Mtume, swallalahu alayhi wasalam, amesema kuwa: «Allah ameandika kufanya uzuri katika kila jambo. Mtakapo ua, ueni vizuri. Na mtakapo chinja, chinjeni vizuri. Na mmoja wenu anoe kisu chake, na ampumzishe mnyama wake aliyemchinje (asimuache akapaparika)». (Muslim, Hadithi Na. 1955).

Siku moja Mtume, swallalahu alayhi wasalam, alihudhuria mazishi ya mtu mmoja akawa anawaelekeza Maswahaba namna ya kurekebisha vizuri mwanandani na kuzika vizuri. Kisha aliwageukia na kuwaambia kuwa: «Ama kwa hakika, jambo hili halimsaidii marehemu na wala halimdhuru. Lakini, Allah anapenda kwa anayefanya jambo akifanya alifanye vizuri».(Baihaqi, Hadithi Na. 5315). Na katika tamko jingine Mtume amesema kuwa: «Allah anapenda mmoja wenu akifanya jambo, alifanye kwa ukamilifu na uzuri».(Abuu yaalaa, Hadithi Na. 4386)..(Tazama tabia njema zilizobaki uk 192)

Mwongozo Mwepesi wa Muislam

Mtandao wa Mwongozo Mwepesi wa Muislam ni kitabu cha Mtandaoni cha kitabu asili ‘Mwongozo Mwepesi wa Muislam’ ambacho ni moja ya mradi wa Kampuni ya Mwongozo wa Kisasa na kimetolewa katika Lugha Zaidi ya 15 na maudhui yake yameambatana na ujuzi mkubwa wa kimtandao katika kufikisha.

الدليل المعاصر