You are here

المحرم لكسبه

2- Ulaghai na kutojua

Makusudio yake ni kila mkataba ambao ndani yake kuna sehemu haijulikani au kuna mwanya ambao unaweza ukawa sababu ya kuleta mzozo na ugonvi kati ya pande mbili au mmoja kumdhulumu  mwengine.

Mkataba huu Uislamu umeuharamisha ili kuziba mwanya wa sababu za ugomvi, dhuluma na kupunjana. Mkataba huu ni haramu hata kama watu watauridhia. Mtume, swallalahu alayhi wasalam, amekataza biashara za ulaghai. (Muslim, Hadithi Na. 1513).

Uislamu unaharamisha kila mkataba (makubaliano) wenye sehemu isiyofahamika ambayo baadae inaweza kusababisha mzozo na ugomvi.

Mfano wa biashara za ulaghai na kutojua

  1. Kuuza matunda kabla ya kukomaa na kuwa tayari kuchumwa. Mtume, swallalahu alayhi wasalam, amekataza kufanya hivyo, kwa sababu ya uwezekano wa matunda hayo kuoza kabla ya kupevuka. 
  2. Kulipa kiasi fulani cha pesa kwa ajili ya kununua sanduku ambalo haijulikani ndani yake kuna nini; inawezekana kukawa na kitu chenye thamani au kitu kisichokuwa na thamani.

Wakati gani kutojua kunakuwa na athari?

Ulaghai na kutojua hakuwi na athari katika kuifanya mikataba kuwa haramu isipokuwa tu utakapokuwa mwingi na ukawa katika mkataba wenyewe na sio katika viambatanishi vyake. Kwa maana hiyo, inafaa kwa Muislamu kununua nyumba, kwa mfano, hata kama hajui, kama vile rangi n.k. Huku ni kutojua kidogo, na pia kutojua huku kupo katika viambatanishi vya mkataba na sio katika mkataba wenyewe.

3- Dhulma na kuchukua mali za watu kinyume na utartibu

Dhuluma ni katika mambo mabaya sana ambayo Uislamu umeyakataza. Mtume, swallalahu alayhi wasalam, amesema kuwa: «Dhuluma ni giza Siku ya Kiama». (Bukhari, Hadithi Na. 2315. Muslim, Hadithi Na. 2579). Kuchukua mali za watu bila ya haki, hata kama ni kidogo, ni katika madhambi makubwa ambayo mwenye kuyafanya ameahidiwa adhabu kali Akhera. Mtume, swallalahu alayhi wasalam, amesema kuwa: «Mwenye kudhulumu kipande cha shubiri ya ardhi, atabebeshwa shingoni kipande cha ardhi hiyo Siku ya Kiama kuanzia ardhi ya saba». (Bukhari, Hadithi Na. 2321. Muslim, Hadithi Na. 1610).

Mifano ya duluma katika miamala:

  1. Kughushi na kulaghai watu kwa ajili ya kula mali zao kwa njia batili. Hayo ni miongoni mwa madhambi makubwa. Mtume, swallalahu alayhi wasalams, amesema kuwa: «Mwenye kutufanyia ghushi si mwenzetu» (Muslim, Hadithi Na. 101). Sababu ya Hadithi hii ni kwamba Mtume, swallalahu alayhi wasalam, alikwenda sokoni na kukuta fungu la nafaka. Aliingiza mkono wake katika fungu hilo la nafaka na kukuta umajimaji humo. Alimuuliza mfanyabiashara kwamba: Ni nini hiki ewe mwenye nafaka hizi? Mfanyabiashara akajibu kuwa: Zimenyeshewa na mvua ewe Mtume wa Allah. Mtume akasema: Kwa nini hukuziweka juu watu wakaziona? Halafu Mtume akasema: Mwenye kughushi si mwenzetu». (Tirmidhiy, Hadithi Na. 1315)
  2. Kuchezea sheria kwa kuchukua mali kwa dhuluma na bila ya haki. Hali hii ni kwamba mtu anaweza kuwa na ujanja na umahiri wa hali ya juu unaomuwezesha kuchukua kitu kisichokuwa chake kwa njia ya sheria na mahakama. Lakini, hukumu ya hakimu hauibadilishi batili kuwa haki, kama alivyosema Mtume, swallalahu alayhi wasalam, kuwa: «Hakuna vingine isipokuwa kwamba mimi ni mwanadamu tu kama nyinyi. Na nyinyi mnaleta mashitaka yenu kwangu. Na huenda mmoja wenu akawa hodari zaidi wa kutetea hoja yake kuliko mwenzake, na kwa sababu hiyo, nikampa hukumu ya ushindi kutokana na nilivyo sikia. Yule ambaye nimempa hukumu ya ushindi kwa haki ya ndugu yake, asiichukue, kwa sababu nitakuwa nammegea kipande cha moto». (Bukhari, Hadithi Na. 6748. Muslim, Hadithi Na. 1713)
  3. Kutenza nguvu (Kushurutisha): Haifai kutenza nguvu katika muamala kwa namna yeyote ile ya ushurutishaji na ukandamizaji. Mikataba haiwi sahihi isipokuwa tu kwa kuridhiana. Mtume, swallalahu alayhi wasalam, amesema kuwa: «Hakuna vingine isipokuwa kwamba  biashara ni kwa kuridhiana». (Ibnumaaja, Hadithi Na. 2185).
  4. Rushwa: Ni mtu kutoa mali au huduma ili apate haki isiyokuwa yake. Rushwa ni miongoni mwa aina mbaya sana za dhuluma na ni miongoni mwa madhambi makubwa sana. Mtume, swallalahu alayhi wasalam, amemlaani mtoa rushwa na mpokea rushwa. (Tirmidhiy, Hadithi Na. 1337)

Rushwa inapoenea katika jamii fulani, jamii hiyo hukumbwa na ufisadi, mvurugiko na kudumaa. 

Mwongozo Mwepesi wa Muislam

Mtandao wa Mwongozo Mwepesi wa Muislam ni kitabu cha Mtandaoni cha kitabu asili ‘Mwongozo Mwepesi wa Muislam’ ambacho ni moja ya mradi wa Kampuni ya Mwongozo wa Kisasa na kimetolewa katika Lugha Zaidi ya 15 na maudhui yake yameambatana na ujuzi mkubwa wa kimtandao katika kufikisha.

الدليل المعاصر