You are here

Nyiradi kubwa zaidi:

Sheria inataka sura za kinga zisomwe kila asubuhi na jioni. Imenukuliwa katika Hadithi kwamba: «Soma (Qul Huwallahu Ahad) na (Qul Auudhu Birabbil Falaq na Qul Auudhu Birabbin-naas) wakati wa asubuhi na wakati wa jioni mara tatu, zitakutosha kwa kukukinga dhidi ya kila kitu». (Tirmidhiy 3575)
Na kila baada ya swala ya faradhi, kama Mtume alivyomfundisha Swahaba mmoja. (Abudaudi 1523)
Na kabla ya kulala. Mtume alipokuwa akipanda kitandani kwake kila usiku alikuwa akiviweka pamoja viganja vyake halafu anatabana humo na kusoma (Qul Huwallahu Ahad) na (Qul Auudhu Birabbil Falaq) na (Qul Auudhu Birabbin-naas), halafu anajipangusa kwa kutumia viganja hivyo sehemu awezazo katika mwili wake akianza kichwa chake na uso wake na sehemu ya mbele ya mwili wake. Anafanya hivyo mara tatu». (Bukhariy 4729)

Sura hizo ni kinga kubwa sana inayomkinga mwanadamu dhidi ya uchawi na uovu. «Mtume alikuwa akiomba kinga dhidi ya majini na macho ya watu mpaka ziliposhuka sura za kinga. Alizitumia sura hizo na kuacha nyinginezo». (Tirmidhiy 2058)

Nyiradi muhimu

Hii ni aya kubwa sana katika Qur’ani kama ambavyo Mtume amelieleza hilo, kwa sababu ya Allah anavyotukuzwa humo na sifa zake kamilifu na uwezo wake mkamilifu unaotajwa humo.

Sheria pia inataka aya hii isomwe asubuhi na jioni na kabla ya kulala. Imenukuliwa katika Hadithi kwamba, mwenye kuisoma aya hii kabla ya kulala ataendelea kuwa katika ulinzi wa Allah na shetani hatamsogelea mpaka asubuhi. (Bukhariy 2187)

Pia inasomwa baada ya swala. Mtume amesema kuwa: «Mwenye kusoma Aya Kursiy baada ya kila swala ya faradhi hakuna kitakachomzuia kuingia peponi isipokuwa kifo tu». (Annisai 9848) 

«Allahu Laa Ilaaha Illaa Huwal-hayyul-qayyuum. Laa Ta’khudhuhuu Sinatun Walaa Nauum. Lahuu Maa Fissamaawaati Wamaa Fil-ardhi. Man-dhalladhii Yashfau Indahuu Illaa Bi-idhnih. Yaalamu Maa Baina Aydii Him Wamaa Khalfahum. Walaa Yuhiitwuuna Bishai-in Min-ilmihii Illaa Bimaa Shaa’a. Wasia Kursiyyuhussamaawaati Wal-ardhi. Walaa Yauuduhuu Hifdhuhumaa Wahuwal-aliyyul-adhwiim». (Sura Albaqara, aya 255)

«Allahu Laa Ilaaha Illaa Huwa»

Allah ni ambaye hakuna anayestahiki kuabudiwa kwa haqi ila yeye tu.

«Alhayyul-qayyuum»

Aliye hai, ambaye yeye tu ndiye mwenye maana zote za uhai mkamilifu unaolingana na utukufu wake, msimamizi wa kila jambo kwa kuliandaa na kulifanya vizuri. 

«Laa Ta’khudhuhuu Sinatun Walaa Nauum»

Hasinzii wala halali.

«Lahuu Mafis-samaawaati Wamaa Fil-ardhi»

Ni vyake yeye tu vyote vilivyomo ulimwenguni; mbinguni na ardhini, kwa sababu yeye ndiye mwenye kuvimiliki.

«Man Dhalladhii Yashfau Indahuu Illaa Bi-idhnih»

Hakuna yeyote atakayekuwa na ujasiri wa kuombea mbele yake isipokuwa kwa idhini yake tu.

«Yaalamu Maa-bayna Aydiihim Wamaa khalfahum»

Anajua mambo yao yajayo na ya zamani yaliyopita.

«Walaa Yuhiitwuuna Bisha-in Min-ilmihii Illaa Bimaa-shaa’a

Hakuna kiumbe yeyote anayejua chochote katika anayoyajua Allah isipokuwa tu yale ambayo Allah amemjuza na kumfahamisha.

«Wasia Kursiyyuhussamaawaati Wal-ardhi»

Baadhi ya wafasiri wamefasiri «Kursiy» kwamba ni mahali ilipo miguu ya Allah kwa namna inayolingana na utukufu wake. Kursiy ni miongoni mwa viumbwa vikubwa vya Allah ambavyo vinazishinda mbingu na ardhi kwa ukubwa na upana.    

«Walaa Ya-uuduhuu Hifdhuhumaa»

Hakumuelemei Allah kuzitunza mbingu na ardhi na vilivyomo humo. 

«Wahuwal Aliyyul Adhiim»

Na yeye kwa dhati yake na sifa zake yuko juu ya viumbe vyake, ni mwenye sifa zote za utukufu na ukubwa.

Mwongozo Mwepesi wa Muislam

Mtandao wa Mwongozo Mwepesi wa Muislam ni kitabu cha Mtandaoni cha kitabu asili ‘Mwongozo Mwepesi wa Muislam’ ambacho ni moja ya mradi wa Kampuni ya Mwongozo wa Kisasa na kimetolewa katika Lugha Zaidi ya 15 na maudhui yake yameambatana na ujuzi mkubwa wa kimtandao katika kufikisha.

الدليل المعاصر